Sunday, June 29, 2025

Mabadiliko ya Sera na Sheria za Uteuzi wa Viongozi na Wagombea wa Nafasi za Uongozi


Elimu na Uongozi: Hoja ya Mabadiliko

✍️ HD Jeyma Maduwa

LL.B. (Hons)

Katika zama hizi za maendeleo ya kasi duniani sayansi, teknolojia, uchumi wa kidigitali na mabadiliko ya kijamii  hatuwezi tena kuamini kuwa kujua kusoma na kuandika pekee kunatosha kumfanya mtu kuwa kiongozi. Uongozi ni zaidi ya uwezo wa kuandika jina lako au kusoma hotuba. Unahitaji maarifa, maono, busara, na weledi wa hali ya juu.

Leo hii, bado tunaona nafasi muhimu za kiuongozi zikishikiliwa na watu wasiokuwa na msingi wa elimu. Je, tunaweza kweli kutarajia mageuzi ya maana katika uchumi, siasa au jamii ikiwa viongozi wetu hawana uelewa wa masuala haya? Viongozi wasio na elimu hawawezi kuelewa changamoto zinazokikabili kizazi cha sasa, wala hawawezi kutunga sera bora au kufanya maamuzi sahihi kwa manufaa ya wananchi.

Kadri tunavyoelekea kwenye uchaguzi mkuu, majina ya watu wanaochukua fomu yanatoa taswira halisi ya hali ilivyo. Kwa masikitiko makubwa, vigezo vya msingi kama elimu, uzoefu au maono hayazingatiwi ipasavyo. Tunashuhudia nafasi za uongozi zikitafutwa kwa kutumia umaarufu wa kisanii, ushabiki wa kisiasa au hata ushawishi wa kifamilia. Hali hii ni hatari kwa mustakabali wa taifa letu.

Na kwa huzuni zaidi, umaarufu umegeuzwa kuwa tiketi ya kisiasa. Mtu akiwa maarufu, hata kama hana mchango wa moja kwa moja kwa jamii, hupewa heshima ya kugombea nafasi nyeti. Umaarufu bila maarifa ni sawa na upofu wa kisiasa. Tusikubali uongozi kuwa ajira ya kawaida au zawadi ya majina makubwa; uongozi ni dhamana inayohitaji ukomavu wa kiakili, elimu, na maadili ya hali ya juu.

Kwa mfumo wa sasa wa sheria, ambapo hakuna masharti madhubuti ya elimu kwa wagombea wa baadhi ya nafasi, tutaendelea kuongozwa kwa kubahatisha. Tutaendelea kulalamika, na mzunguko wa viongozi wasio na dira utaendelea kutugharimu maendeleo yetu kama taifa.

Ni kweli kwamba kujua kusoma na kuandika ni msingi, lakini hiyo haitoshi kabisa. Taifa linahitaji viongozi walioelimika, wenye uelewa mpana wa muktadha wa kisiasa, kijamii na kiuchumi. Uongozi usichukuliwe kama kazi ya kawaida bali kama wito wa kweli wa huduma kwa wananchi. Kiongozi wa kweli ni yule anayebeba maono ya maendeleo na anayejua anapoelekea.

Elimu ni dira. Ni silaha dhidi ya ujinga na upofu wa kiuamuzi. Taifa lolote linalothamini maendeleo lazima liweke elimu mbele — si kwa wananchi tu, bali pia kwa viongozi wake. Uongozi si urithi wa kifamilia wala tuzo ya kisiasa. Ni wajibu unaohitaji maandalizi makini na mwelekeo wa dhati.

Ni wakati wa kufanya mabadiliko ya kisheria. Sheria yetu ihakikishe kuwa wagombea wa nafasi za uongozi wana kiwango cha chini cha elimu kinachowapa uwezo wa kuongoza kwa ufanisi. Tusipochukua hatua sasa, tutazidi kuona taifa likiongozwa pasipo dira, na matokeo yake ni taifa lisiloelekea popote salama.

Uongozi usio na elimu ni sawa na jahazi lisilo na nahodha hatuwezi kufika salama.

#MaarifaKwanza #UongoziBora #ElimuNdiyoNguzo



No comments:

Post a Comment

Mabadiliko ya Sera na Sheria za Uteuzi wa Viongozi na Wagombea wa Nafasi za Uongozi

Elimu na Uongozi: Hoja ya Mabadiliko ✍️ HD Jeyma Maduwa LL.B. (Hons) Katika zama hizi za maendeleo ya kasi duniani sayansi, teknolojia, uchu...